TANZANIA HAITAUZA MENO YA TEMBO

Posted by Arusha by day and by night On 00:13 No comments





Pascal Shelutete,
TANAPA

Serikali ya Tanzania haitawasilisha maombi ya kuuza akiba yake ya meno ya tembo kwa Chombo cha Kimataifa chenye jukumu la kusimamia Biashara ya Wanyamapori na Mimea ambao wako hatarini kutoweka (CITES) ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Kimataifa za kupiga
marufuku biashara haramu ya meno ya tembo duniani. 

Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu ameyasema hayo jijini London, Uingereza
anakohudhuria Mkutano wa Kimataifa unaohusu Biashara Haramu ya Wanyamapori duniani.

Waziri Nyalandu alisema kuwa uamuzi huo wa Serikali ulifikiwa tangu mwishoni mwa mwaka jana baada ya serikali kusaini harakati za Taasisi ya Mke wa Rais wa zamani wa Marekani Hillary Clinton inayofahamika kama Clinton Global Initiative inayopigania kupigwa marufuku kwa biashara ya
meno ya tembo duniani.

Akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa na Tanzania katika vita dhidi ya ujangili, Waziri Nyalandu alisema kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana watuhumiwa 320 kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya, China, Afrika na Tanzania wamekamatwa wakihusishwa na biashara ya meno ya tembo na
kuwa wameshafikishwa katika vyombo mbali mbali kwa ajili ya hatua za
kisheria.

Aidha, Waziri Nyalandu alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, tani 19.7 za meno ya tembo zilikamatwa katika maeneo mbali mbali duniani na kati ya hizo tani 15.2 zilikamatwa na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na vyombo mbalimbali ikiwemo Jumuiya ya Kimataifa.

Kuhusiana na mafanikio ya sekta ya uhifadhi nchini, Nyalandu alibainisha kuwa Hifadhi Taifa ndizo salama zaidi kwa maisha ya wanyama katika Bara la Afrika kwa sasa na hasa kutokana na takwimu kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita idadi ya tembo waliouawa katika Hifadhi ya Serengeti
ilipungua kutoka wastani wa tembo watatu kwa mwezi hadi sifuri na kwamba ndiyo nchi yenye faru weusi kwa wingi zaidi katika bara la Afrika.

Waziri Nyalandu alibainisha kuwa serikali iko katika maandalizi ya kufanya sensa kubwa ya kitaifa itakayobainisha idadi halisi ya tembo nchini na kuwa sensa zilizofanyika hivi karibuni katika mifumo ya kiikolojia ya Selou- Mikumi na Ruaha-Rungwa zililenga kutoa picha ya awali ya idadi ya wanyama hao nchini. 

Katika sensa hizi zilibaini uwepo wa tembo 13, 084 katika mfumo wa kiikolojia wa Selou-Mikumi na zaidi ya 20,000 katika mfumo wa Ruaha-Rungwa idadi ambayo ni zaidi ya wale wanaopatikana
katika nchi jirani ya Kenya.

0 comments:

Post a Comment