MGOGORO WA SHAMBA LA NKWANSIRA WILAYANI HAI

Posted by Arusha by day and by night On 21:01 No comments



TAARIFA YA SHAMBA LA NKWANSIRA

Shamba hilo linalomilikiwa na vyama sita vya msingi liliingia katika mgogoro mkubwa baada ya kukodishwa kwa kampuni moja inayoitwa Agromasters.

Mgogoro huo ulikuwa mkubwa zaidi Mnamo mwezi wa Septemba 2013 baada ya wananchi wa vijiji husika kuvamia shamba.

Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Hai ililazimika kuingilia na kuagiza kusimama kwa mwekezaji wa Agromasters kutumia shamba mpaka hapo taratibu za uendeshaji na kuweka uongozi unaotambulika utakapokamilika na shamba lilikuwa chini ya uangalizi wa Kamati za maendeleo za kata.

Kwanini kamati hiyo iliingilia ? Ilifanya hivyo kutokana na majukumu ya msingi ya kamati ya kusimamia masuala ya ulinzi na usalama ya kila siku katika wilaya na kwa upande wa shamba hilo kulionekana wazi mazingira ya kutokea kwa kuvunjika kwa amani.

Taratibu za ushirika zilifanyika na wanachama walichagua na kuweka uongozi ambao mapema mwezi uliopita kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ilikwenda kuwakabidhi shamba ambalo kwa muda wote lilikuwa likilindwa na kamati za maendeleo za kata za Masama kati na Masama Magharibi.

Kazi ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ilikoma hapo na kuwataka sasa viongozi hao waendelee na mchakato wa kuhakikisha kwamba shamba linaendeshwa kwa ufanisi zaidi.

Hata hivyo haikupita wiki mbili viongozi hao walikuja tena wilayani na kulalamika kwamba katika shughuli yao wanapata vikwazo na changamoto nyingi ikiwemo kukosa ushirikiano wa makabidhiano kutoka kwa vongozi waliokuwa wanaendesha shamba hilo.

Lakini la pili walieleza kuwa walimwita mwekezaji aliyewekwa shamba na kutaka kujua kwa kina mikataba yakena  mwekezaji huyo aliwaeleza wazi kama wanataka kutangaza zabuni ya kumpata mwekezaji mpya lazima kwanza wamlipe fedha zake alizotumia kuwekeza shambani hapo kiasi cha shilingi milioni 200.

Lakini la tatu mwekezaji huyo aliwaeleza wazi kwamba kama kutakuwa na mazingira yoyote ya kutaka kumdhulumu kile alichowekeza inatamlazimu kwenda mahakamani.kama ilivyo kawaida tuliyozoea na hapa Hai mifano ipo kwa mashamba ambayo sasa ni miaka kumi hayajaweza kutumika kutokana na kuwa katika kesi kama Silverdare na shamba la Lambo vivyo hivyo lengo la shamba la Nkwansira lilielekea katika kuweka zuio la mahakama yaani Curviet la kutotumika kwa shamba mpaka kesi ya msingi itakapoisha.

Mazingira yanafanana sana mfano pale Lambo,mwekezaji kampeni inayoitwa SHITECO haikuwa na mkataba na ilikataliwa na wanachama baada ya kuingizwa shambani na bodi nay eye kukimbilia mahakamani na kesi ipo mahakamani tangu mwaka 2005 na hivyo hivyo kwa shama la Silverdare ambapo Benjamini Mengi alifungua kesi baada ya kuondolewa shambani na uongozi wa shamba.

Kama kamati ya Ulinzi ya wilaya tulilazimika kuwaita viongozi wa zamani ambao kwa idadi ni Arobaini na mbili pamoja na viongozi wa joint na mwekezaji ili kufahamu ukweli halisi wa suala hilo.

Kwanza tuliweka sawa tatizo la kuingizwa kwa mwekezaji kwamba halikufuata taratibu zote zinazotakiwa ambazo ni kupata Baraka kutoka kwa wanachama wote.Viongozi wa zamani walikiri hilo.

Lakini la pili ilikuwa kuwapatanisha viongozi wa zamani na wa sasa ili kuwata ushirikiano utakaowezesha kufahamu hali ya shamba tangu kutoka kwa marehemu Ghigas mpaka sasa,nini kilichoachwa na nini kilichopo kisheria.

Kufahamu mkataba uliopo kati ya mwekezaji aliyeingizwa shambani na uongozi uliopita.

Baada ya hapo tuliwashauri uongozi halali wa shamba sasa uendelee na mikutano mfululizo huko shamba kwa ajili ya kumaliza suala la uendeshaji wa shamba,sisi kama kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hatuhusiki kwa lolote lile kwani uamuzi wa mwisho ni wanachama wenyewe.

Lakini kubwa zaidi katika masuala ya ushauri,kamati ya ulinzi na usalama ilifikia maamuzi suala hilo sasa kama viongozi hao watahitaji ushauri wa kitaalamu mfano wa ushirika,sheria,zabuni na kilimo wawasiliane na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hai ambaye ndiye kimsingi mwenye jukumu na mamlaka ya kusimamia shughuli za maendeleo za wilaya.

Kwa masuala ya usimamizi wa ushirika kisheria hayaingiliwi na viongozi wa serikali,bali sheria inatoa mamlaka kwa Mrajisi msaidizi wa Mkoa ambaye yupo mjini Moshi na hatua inayofuata ni mrajisi wa ushirika aliyepo Dodoma na mwisho kwa waziri husika.

HITIMISHO:Kutokana na taratibu na sheria za uendeshaji wa ushirika,hakuna hatua yoyote ya uendeshaji wa shamba hilo itakayofanyika bila ya kupata Baraka ya wanachama wote kwa maana mkutano mkuu.

Msisitizo mkubwa kwa viongozi wapya ili matatizo yaliyojitokeza yasijirudie,wahakikishe shughuli zao wanaendesha kwa uwazi mkubwa wasiruhusu minong’ono kutawala,kwa kila hatua ni vyema wanachama waelewe na kuafiki.

0 comments:

Post a Comment