Na Richard Mwangulube,Hai
Wenyeviti wa vitongoji na vijiji wapatao 116 katika wilaya ya Hai wameondoa tishio lao la kutoshiriki katika sensa na kuahidi kushirikiana na makarani wa zoezi katika kuhakikisha linafanikiwa
Wenyeviti hao walitoa tishio hilo kwa barua kwenda kwa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Hai na kumkabidhi nakala mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama alipokuwa katika ziara ya kuhamasisha sensa wilayani Hai Jumanne iliyopita.
Wenyeviti hao walifuta mpango huo baada ya kuwa na klikao cha saa mbili na mkuu wa wilaya ya Hai Novatus Makunga na kuahidi kuwaongoza makarani wa sensa katika vitongoji vyao
Kaimu mwenyekiti wa umoja wa wenyeviti wa vitongoji wilayani Hai Simon Mnyampanda ameeleza kuwa baada ya kikao hicho na mkuu wa wilaya ya hai, Makunga sasa wamepata ari na nguvu ya kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa.
Tamko hilo ambalo limesainiwa na wenyeviti wapatao 103 kwenda kwa mkuu wa wilaya na nakala kwa mkuu wa mkoa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya wameeleza kwa kauli moja wanafuta tamko lao la awali ambalo lilikuwa likieleza kuwa hawatajihusisha na kuwaongoza makarani kwa zoezi la sensa katika vitongoji vyao kwa kuwa hawajuhi mipaka na ukomo wao na sheria na kanuni za sensa.
Naye mkuu wa wilaya hiyo,Novatus Makunga aliwataka wenyeviti hao kabla ya kushiriki katika zoezi hilo kufuta tamko lao kwa maandishi agizo ambalo walilikubali na baadaye kukutana na kutoa waraka wa kufuta tamko la awali la tarehe 17/08/2012 la kutowaongoza makarani wa sensa.
Baada ya kukubali kuliondoa na kulifuta tamko lao,Makunga aliwaagiza waratibu wa sensa wilayani humu kuwagawia nyaraka na vipeperushi mbalimbali vinavyohusu sensa na pia aliwafafanulia kuwa katika kazi hiyo tayari ofisi ya taifa ya takwimu imetoa muongozo wa wenyeviti hao kulipwa posho maalumu ya kuwaongoza makarani
Wenyeviti hao walitangaza kususia zoezi la sensa wakishinikiza kulipwa posho zao za jumla ya shilingi milioni 280 wanazodai kwamba halmashauri ya wilaya hiyo haijawalipa tangu mwaka 2008
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama kutokana na barua hiyo aliwapa siku moja wenyeviti hao kuandika barua ya kujitoa katika ushiriki wa zoezi hilo endapo msimamo wao unabaki pale pale wa kutotoa ushirikiano kwa makarani wa sensa
0 comments:
Post a Comment