Na Richard Mwangulube,Hai
Mwenge wa uhuru utakuwa wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Kesho jumapili Agosti 5,2012 kuanzia mapema asubuhi na kukesha mpaka jumatatu kabla ya kuendelea na mbio zake katika wilayani Siha.
Kwa mwaka huu wa 2012,mwenge wa uhuru utaweza kupitia jumla ya miradi mitano ambapo kati ya miradi hiyo mmoja utazinduliwa na mwingine utafunguliwa wakati miradi mingine mitatu itawekewa mawe ya msingi.
Miradi hiyo ina jumla ya thamani ya shilingi 311,076,808.Katika miradi hiyo mchango wa serikali kuu ni shilingi 100,000,000,halmashauri ya Hai shilingi 80,369,665 huku nguvu za wananchi zikiwa shilingi 24,274,443 ilhali wahisani wakichangia shilingi 106,432,710.
Mradi wa kwanza utakuwa wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa zahanati ya Shirimgungani itakayokuwa na uwezo wa kuishi watumishi wawili na tayari imeshapauliwa na imegharimu shilingi milioni 23,991,433.
Mradi mwingine ni wa bwalo katika shule ya msingi ya Kimashuku ambapo jengo limepauliwa na gharama ya ujenzi ni shilingi 60,000,000.
Mradi mwingine ni ujenzi wa vyumba vya madarasa matatu ya sekondari ya maili sita.Ujenzi wa Madarasa hayo yote matatu umekamilika na yamegharimu jumla ya shilingi 62,352,665.
Mradi mwingine wa Chama cha Ushirika wa kuweka na kukopa(Saccos) ya MUVIMAHA na TALANTA ambapo jengo limekamilika na mradi umegharimu kiasi cha shilingi 50.732,710.
Mradi wa mwisho ni ujenzi wa wodi ya upasuaji katika hospitali ya wilaya ya Hai ambapo jengo lipo kwenye hatua ya kupauliwa na limegharimu shilingi 114,000,000.
Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga atapokea mwenge katika ofisi za kijiji cha Shirimgungani majira ya saa tatu asubuhi kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Moshi,Dk Ibrahimu Msengi.
Mkesha wa Mwenge wa uhuru utakuwa katika uwanja wa michezo wa mji wa Bomang’ombe ambapo kutakuwa na burudani mbalimbali zikiwemo za muziki wa kizazi kipya yaani Bongo fleva na muziki wa dansi zikiwemo nyimbo zilizovuma enzi za zamani.
Mbio za Mwenge wa uhuru kwa mwaka huu zimebeba ujumbe ufuatao;Sensa ni msingi wa mipango ya maendeleo yetu,shiriki kuhesabiwa tarehe 26,Agosti 2012,mabadiliko ya katiba jitokezeni kutoa maoni yako,mapambano dhidi ya ukimwi na dawa za kulevya na rushwa
Mkuu wa Wilaya ya Hai,Novatus Makunga akishiriki katika upokeaji wa Mwenge wa Uhuru ulipoingia mkoani Kilimanjaro mnamo Julai 31,2011
Kiongozi wa wakimbiza mwenge wa Uhuru 2012,kapteni Honest Ernest Mwanossa akihojiwa na waandishi wa habari mara tu baada ya mwenge wa uhuru kuingia mkoani Kilimanjaro ukitokea mkoani Manyara
0 comments:
Post a Comment