MBWA HATARI KIJIJI CHA NKWANSIRA KUUAWA KABLA YA IJUMAA

Posted by Arusha by day and by night On 02:03 No comments



Na Richard Mwangulube,Hai

Serikali wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro kimemuamuru mwananchi mmoja wa kijiji hicho anayemiliki kundi la mbwa ambao wamekuwa tishio kwa wananchi awaue kabla ya kufikia Ijumaa ijayo Agosti 15 ya mwezi huu.

Hatua hiyo ilifikiwa kutokana na  agizo la mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga kwa afisa wa mifugo wa wilaya hiyo kufuatia kero ya muda mrefu ya wananchi wa kijiji hicho kushambuliwa na baadaye kung’atwa na mbwa hao iliyowasilishwa na mwananchi Elingaya Tarimo.

Makunga ameeleza kuwa Afisa Mifugo wa wilaya,Fratern Augustin Mtika amekamilisha kazi hiyo kwa kukutana na mmiliki wa mbwa hao aliyemtaja kwa jina la Afraeli Mbise pamoja na wananchi mbalimbali ambao kwa nyakati tofauti waliumwa na mbwa hao.

Amesema kuwa mtuhumiwa huyo anafuga mbwa watano nyumbani kwake bila kuwa na nyumba inayokidhi matakwa ya sheria ya kufuga mbwa ambayo inaelekeza makazi hayo lazima yawe yamezungushiwa uzio ambao mbwa hawawezi kutoka nje na kuleta madhara.

Makunga ameeleza kuwa afisa huyo wa mifugo aliitisha kikao cha pamoja kati ya mwenyekiti wa kitongoji cha Nkwansira kati,Adolf Masawe,Mfuga mbwa,Afraeli Mbise pamoja na wananchi sita ambao waliumwa na mbwa kwa nyakati tofauti.

Wananchi hao ni pamoja Rose Masawe,Ndenaike Kimaro,Minafyaula Masawe na Tumaini Lema pamoja na wazazi ambao watoto wao waling’atwa na mbwa Jamika Samiyekawake na Martha Phelemon.

Ameeleza kuwa katika kikao hicho walalamikaji walianza kutoa maelezo yao kuhusu walivyong’atwa na mbwa kila mmoja kwa kadiri alivyoweza kujieleza.

Ameeleza kuwa mbwa hao walianza kung’ata watu kuanzia mwezi Julai 2013 na mtu wa mwisho aling’atwa mwishoni mwa mwezi uliopita.Idadi kubwa ya watu waliong’atwa na mbwa hao ni majirani wanaomzunguka mwenye mbwa.

Mkuu huyo wa wilaya ameeleza mfugaji huyo wa mbwa alishindwa pia kuzingatia muda wa kisheria wa kufungua mbwa ambao ni saa nne usiku na kuwafungia saa kumi na moja alfajiri.

Wananchi wote hao waliong’atwa na mbwa walitibiwa vidonda na kuchomwa chanjo ya kuzuia kichaa cha mbwa  kwa gharama zao mwenyewe
.
Kwa upande wake mmiliki wa mbwa hao,Mbise alieleza kuwa kwa kawaida yeye anatoka muda wa usiku sana kwenda kwenye biashara yake ya kuchinja ng’ombe na alikiri kuwa watoto wake ndiyo wanaozembea kufungua na kufunga mbwa kwa muda uliopangwa kisheria.

Hata hivyo Mbise aliwaomba radhi waathirika wote juu ya madhara waliloyapata na wote walimsamehe pamoja na gharama za matibabu na chanjo walizojigharamia kwa moyo mmoja na kumsisitiza waendelee kuishi vizuri kama majirani wema.

Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kuwa zoezi hilo la kuwaua mbwa hao litafanyika chini ya usimamizi wa mwenyekiti wa kitongoji na mgambo wa kijiji na kwamba afisa huyo ya mifug wa mifugo atakwenda kukagua na kuthibitisha kuuawa kwa mbwa hao Jumatatu ijayo Agosti 18 mwaka huu

0 comments:

Post a Comment