Na Mwandishi Wetu,Hai
Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga amesema
kwamba njia pekee ya kutatua matatizo katika sekta za kilimo na mifugo ya
ubora,ufungashaji na uzalishaji unaotimiza mahitaji ya soko ni kuhakikisha
jitihada zinaelekezwa katika kuziba pengo la kiteknolojia katika kilimo na
ufugaji
Makunga ametoa wito huo wakati alipofanya ziara
ya kutembelea shamba darasa la kijiji cha Roo pamoja na kuongea na wakulima wa
vikundi viwili vya umoja na upendo vinavysimamia
shamba hilo ikiwa ni sehemu ya kuanza kwa wiki ya maadhimisho ya sherehe za
wakulima na wafugaji nchini yaani Nane nane.
Ameeleza kupitia mpango huo wa mashamba
darasa,umeweza kuziba pengo hilo la kiteknolojia katika kilimo kutokana na
idadi kbwa ya wakulima katika kijiji hicho kuanza kulima kilimo chenye tija
ambacho sasa kinatoa mwelekeo wa kujikomboa kiuchumi.
Makunga ametoa mfuno wa aina ya kilimo cha
migomba ambacho kinatumika sasa hivi cha migomba mifupi ambacho katika shamba
moja kina uwezo wa kumpatia mkulima mikungu ya ndizi ipatayo 1350 ambapo kwa
mavuno yanayochukuwa miezi kumi na mbili ana uwezo wa kutengeneza shilingi
milioni 13.5 kwa kuuza kwa bei ya chini ya shilingi 10,000.
Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kupitia mashamba
hayo darasa wakulima wanapata mbegu za aina hiyo ya migomba kutokana na
machipukizi kila baada ya miezi mitatu na kwenda kuotesha katika mashamba yao.
Aidha Makunga ameeleza kufarijika na kilimo cha
mihogo kwa kutumia matuta kuanza kushika kasi katika eneo hilo la nyanda za
kati na juu ambapo kihistoria lilikuwa halilimwi kabisa mihogo kwa kuamini
kwamba ni sumu.
Ameeleza kuwa mbali na mihogo pia wananchi wa
eneo hilo wanalima kwa ufanisi mkubwa viazi vitamu pamoja na majani ya kulishia
mifugo hususani ng’ombe na mbuzi pamoja na kufuga aina ya kisasa ya mbuzi ambao
katika soko huuzwa zaidi ya shilingi 400,000.
“Mpango huu wa uenezi wa miradi wilayani Hai
yaani Spreading Hai tuliuanza mwezo Oktoba mwaka jana chini ya kaulimbiu ya
Njaa na umasikini kuwa historia wilayani Hai inawezekana,hivi sasa umeonyesha
mafanikio makubwa katika vijiji vya Kawaya,Roo,Mungushi na Mulama na lengo ni
kuhakikisha unasambaa katika vijiji vyote ifikapo Oktoba 2014.
Katika risala yao,wakulima hao waliomba serikali
kuwapatia pembejeo za kilimo kwa wakati muafaka na kumwomba mkuu huyo wa wilaya
kuwa mlezi wa vikundi vyao viwili vya umoja na upendo.
0 comments:
Post a Comment