DC HAI AWATAKA WANANCHI KUWACHARUKIA WACHAKACHUAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

Posted by Arusha by day and by night On 05:59 No comments

Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga akizungumza katika mkutano wa kijiji cha Mbatakero
Diwani wa kata ya Machame kusini,Nasibu Mndeme akizungumza katika mkutano wa kijiji cha Mbatakero
Wananchi wa kijiji cha Mbatakero wakifuatilia mkutano wao wa kijiji
Wananchi wa kijiji cha Mbatakero wakifuatilia mkutano mkuu wa kijiji
Wananchi wa kijiji cha Mbatakero katika mkutano wa kijiji


Na Richard Mwangulube,Hai

Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga ametoa wito kwa wananchi kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi mbalimbali kuanzia hatua ya awali mpaka pale inapokamilika na endapo katika hatua Fulani watapatwa na wasiwasi wa viwango vinavyotakiwa wawasiliane na viongozi wa juu.

Makunga ametoa wito huo katika mkutano mkuu wa kijiji cha Mbatakero kilichopo katika kata ya Machame Kusini ambapo wananchi wa kijiji hicho wakitoa kero zao walibainisha kutoridhishwa na ukarabati wa barabara inayoanzaia kijiji cha Kwasadala hadi kijijini kwao.

Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kuwa hivi sasa kila mwananchi imefikia wakati wa kubadilika na kuondokana na dhana kwamba miradi ya jamii inayotekelezwa katika maeneo yao ni mali ya serikali.

“Nimefurahishwa kukerwa kwenu na ukarabati wa kila mwaka wa barabara ya Kwasadala hadi  Mbatakero,hicho ndicho tunachotaka na kila tunapoenda tunatoa nambari za simu,mimi na mkurugenzi wa halmashari ya wilaya ili mtupe taarifa pale mambo yanapoenda kombo,”alifafanua.

Kwa upande wake,diwani wa Machame Kusini,Nasibu Mndeme aliwaomba wananchi hao wampe wiki moja ya kushughulikia tabia ya kuwekwa hovyo kwa matuta ya barabarani katika barabara hiyo ya changarawe na hivyo kuwa chanzo za ajali hasa kwa wanaotumia boda boda.
 
Aidha Makunga ameeleza moto huo ni lazima kuenea katika miradi yote ikiwemo ya ujenzi wa shule na zahanati pamoja na usambazaji wa maji safi kwa lengo la kudhibiti mianya kwa watu wenye tabia ya kuchakachua fedha za umma na kusababisha ubovu kutambulika siku ya kuzindua miradi husika.

Akizungumzia hali ya ukarabati wa barabara Makunga ameeleza kuwa katika mwaka huu wa fedha serikali kupitia mfuko wa barabara kwa ajil ya kutekeleza kazi mbalimbali za barabara imetenga jumla ya shilingi 1,026,433,150.

Amesema kati a fedha hizo,kiasi cha shilingi 357,000,000 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mnepo ambalo ni kiungo muhimu sana kati ya wilaya ya Hai na manispaa ya moshi.

Makunga ameeleza kuwa halmashauri ya wilaya ya Hai kupitia vyanzo vyake pamoja na nguvu za wananchi watachangia kiasi cha shilingi 30,000,000 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hususani za vijijini

Aidha Halmashauri ya wilaya kupitia mapato yake tangu mwaka wa fedha uliopita ilianza kutenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kujenga kilometa moja ya barabara ya lami kila mwaka

Makunga ameeleza kuwa wilaya ya Hai ina mtandao wa barabara zenye jumla ya urefu wa kilometa 471.5 ambapo kati ya hizo kilometa 32 ni barabara za kitaifa na kilometa 27.5 ni barabara za mkoa

0 comments:

Post a Comment