WAHAMIAJI HARAMU WALIOTOROKA MOSHI WAKAMATWA HAI

Posted by MK On 03:04 No comments






Na Richard Mwangulube,Hai

Vyombo vya usalama wilayani Hai mkoani Kilimanjaro vimefanikiwa kuwanasa Wahabeshi wiwili ambao wanadhaniwa ni sehemu ya kundi la wahamiji haramu wanne waliofanikiwa kuwatoroka polisi usiku wa kuamkia ijumaa iliyopita katika eneo la Kilemapofu wilayani moshi.

Wahamiaji haramu hao kutoka Ethiopia walikamatwa jana saa mbili na nusu asubuhi wakiwa wamejificha katika kichaka kichopo katika eneo la Uzunguni katika mji wa Hai maarufu kama Bomang’ombe.

Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga alithibitisha kwa njia ya simu kukamatwa kwa Wahabeshi hao ambapo ameeleza kuwa moja kati ya hao alikuwa na pasi ya kusafiria ya Ethiopia huku mwingine akiwa hana

Alisema kuwa katika maelezo ya awali Wahabeshi hao wamedai kuwa walitelekezwa katika eneo hilo la uzunguni na pikipiki zinazofahamika kwa jina maarufu kama bodaboda huku wakiwa hawaelewi uelekeo wa sehemu walipokuwa wameachwa.

“Tumekuwa na kampeni ya muda mrefu ya kuielimisha jamii kuhusiana na wimbi la sasa la wahamiaji haramu ama kuwepo na biashara haramu ya kusafisha watu kutoka Ethiopia na Somalia,hivyo wananchi walitupa taarifa kuhusiana na kuwatilia wasiwasi watu wawili na baadaye vyombo vya dola vilifanikiwa kuwatia mikononi lakini kikubwa kama wameanza kutumia pikipiki ni vyema tukawa macho zaidi,”alisema Makunga.

Aliwataja Wahabeshi hao kuwa ni pamoja na Tarekegn demeke[21] ambaye alikuwa na pasi ya kusafiria na Alem mituku[25] ambaye hakuwa na pasi ya kusafiria.

Makunga ameeleza kuwa vyombo vya dola wakiwemo polisi na maofisa wa uhamiaji wanaendelea kuwahoji kabla ya kuwachukulia hatua za kisheria zinazosimamia masuala ya uhamiaji.

Ameeleza kuwa kuna kila ushahidi kuwa wahabeshi hao ni sehemu ya kundi la wahamiaji sita waliokamatwa saa tisa usiku wa Septemba sita mwaka huu wilayani Moshi wakiwa wamebebwa na pikipiki tatu wakitokea wilayani Rombo huku lengo likiwa kufika Hai.

Ameeleza kuwa katika tukio hilo wahamiaji wanne walifanikiwa kutoroka huku polisi ikifanikiwa kuwatia mbaroni wawili na madeareva wa pikipiki hizo.

Makunga ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama katika wilaya ya Hai ameendelea kutoa wito kwa wananchi na viongozi wa vijiji kuhakikisha wanatoa taarifa za nyendo zozote za watu wasiofahamika kutokana na wahamiaji hao kubuni njia mpya ya kutumia usafiri wa pikipiki.

Mwishoni mwa wiki hii jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro lilifanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu kumi kutoka Ethiopia pamoja watu saba na pikipiki nne kwa tuhuma za kuwasafirisha wahamaiaji hao katika eneo la Kilemapofu na Mjohoroni wilayani Moshi

0 comments:

Post a Comment