UJENZI WA MAABARA ZA MASOMO YA SAYANSI,MADAWATI NA SHULE MAALUMU WILAYANI HAI

Posted by Arusha by day and by night On 05:13 No comments



HALMASHAURI YA WILAYA YA HAI

MIKAKATI YA UJENZI WA MAABARA ZA MASOMO YA SAYANSI, MADAWATI NA SHULE MBILI MAALUM ZA SEKONDARI

1.0    UTANGULIZI

Halmashauri ya Wilaya ya Hai inazo Shule 45 za sekondari – Shule za serikali ni 29 na Shule zisizo za serikali ni 16 tu zenye usajili.  Kati ya Shule 29 za Serikali ni shule mbili tu – Lyamungo (wavulana tu) na Machame (wasichana tu) – ndizo zenye kidato cha tano na sita.  Shule za sekondari 29 za serikali hadi mwezi Agosti 25, 2014 zilikuwa na jumla ya wanafunzi 11437 – wanafunzi 10019 wa shule za kutwa (Kidato cha I – IV) na wanafunzi 1418 wa shule mbili za Bweni (Kidato cha V – VI).

Aina ya Shule
Wavulana
Wasichana
Jumla
Kutwa (Kidato I – IV)
4686
5333
10019
Bweni (Kidato V – VI)
922
496
1418
Jumla
5608
5829
11437

Yapo maelekezo ya Mkoa na Taifa kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2014, kila Wilaya iwe imetekeleza yafuatayo:
v  Kujenga au kuimarisha maabara za masomo ya sayansi kwa shule zote za Serikali – Wilaya ya Hai zipo shule 29 tu. 
v  Kuteua shule mbili na kuendeleza miundombinu yake, ambazo zinatakiwa kuwa shule maalum na za mfano kwa masomo ya sayansi kwa wilaya – shule ya wasichana na shule ya wavulana.
v  Shule zote za Msingi na Sekondari zisiwe na upungufu wa madawati.

2.0      HALI YA MAABARA SHULENI NA MIKAKATI YA UJENZI WAKE

2.1      Hali ya Uwepo wa Maabara Katika Shule za Sekondari

Halmashauri ya wilaya ya Hai katika shule zake 29 za sekondari inao uhaba mkubwa wa maabara halisi ambapo ni shule nane (8) tu zenye maabara halisi na shule 19 zinatumia vyumba vilivyoboreshwa “Science Rooms” kufundishia masomo ya sayansi kwa vitendo (Science practicals).  Shule sita tu zilipewa “Mobile Laboratories” kwa ajili ya masomo ya Sayansi kwa vitendo (Kiambatisho “A”, “B” na “C”).  Pamoja na upungufu mkubwa wa maabara halisi za sayansi bado wanafunzi wa shule zetu wanasoma masomo ya Sayansi kwa vitendo (Science practicals) na hata kufanya mitihani yao ya mwisho ya kidato cha IV na cha VI kwa vitendo (Real Practicals) na sio “Alternative to Practicals”.  Hatua hii inastahili pongezi kwa Halmashauri, walimu na wanafunzi wetu.

2.2    Mikakati ya Uboreshaji na Ujenzi wa Maabara Shuleni 

Halmashauri ya Wilaya ya Hai katika kutafsiri maelekezo ya Mkoa na Taifa inapendekeza hatua za dharura zifuatazo zichukuliwe ili kujenga maabara mpya, kuboresha vyumba vya madarasa maalum (Science Rooms) na kukamilisha ujenzi wa maabara kwa baadhi ya shule unaoendelea:

Ø  Kila jamii ya shule ielekezwe kujenga maabara moja itakayotumika kwa masomo yote matatu “Multipurpose Laboratory” sawa na ramani iliyopendekezwa na kutolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (WEMU).  Maabara ya aina hii inaaminika kuwa ya gharama ndogo ukilinganisha na maabara ya vyumba vitatu tofauti.  “Multipurpose Laboratory” inakisiwa kutumia kiasi cha Tsh. 45,000,000.00 hadi kukamilika ikiunganishwa na nguvu kazi za wananchi (Kiambatisho “D”);
Ø  Kila jamii ya shule husika isiyo na maabara halisi wamelekezwa kuimarisha vyumba maalum vinavyotumika (science rooms) kwa kujenga miundombinu ya kimaabara ndani ya chumba husika ili kiwe na sifa ya “Multipurpose Laboratory” kwa kuanzia;
Ø  Kuhimiza na kuhamasisha jamii za shule kukamilisha ujenzi wa maabara unaoendelea katika baadhi ya shule kwa kuendesha harambee na michango ya hiari kwa wadau wote wa elimu katika maeneo yao;
Ø  Ofisi ya Mkuu wa Wilaya iunde “Task Forces” zitakazohusisha Kamati ya Ulinzi na Usalama (W) na Watendaji wa Halmashauri zitakazofuatilia ikiwa Viongozi wa Kata na vijiji wanachangisha michango na ujenzi unasimamiwa ipasavyo siku hadi siku kwa kila shule husika;
Ø  Asilimia 30 za mapato ya ndani yaliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitatumika kujengea maabara;
Ø  Fedha za CDG kwa mwaka 2014/2015 za vijiji zinaelekezwa kuimarisha vyumba vya maabara.
3.0      UIMARISHAJI WA SHULE MBILI MAALUM ZA WILAYA

3.1      Sifa za Shule Mbili Maalum Zinazotakiwa

Maelekezo ya Mkoa juu ya kuteua shule mbili – wasichana na wavulana – ambazo zitakuwa maalum kwa wanafunzi maalum (wenye ufaulu wa juu ndani ya wilaya kwa Mtihani wa kuhitimu Darasa la VII), yametoa sifa zifuatazo kuzingatiwa:
*      Shule iwe na eneo la kutosha (sio chini ya ekari 5) ili kuruhusu upanuzi wa shule kwa kujenga miundombinu muhimu kwa shule yenye bweni/hosteli;
*      Kuwepo na shule nyingine jirani ili kuweza kuchukua wanafunzi wa Kata/vijiji husika ambao ufaulu wao hautafikia kiwango cha kuingia shule maalum ya jirani;
*      Shule iwe na mazingira ya kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii;
*      Shule zitakuwa ni za michepuo ya Sayansi – zitaweka mkazo zaidi katika masomo ya sayansi na Hisabati.

3.2.      Maamuzi ya Halmashauri ya Wilaya

Halmashauri ilipopitia sifa zilizoainishwa katika kipengele 3.1, imejiridhisha na shule mbili za sekondari – Kia na Mukwasa – kuwa zinastahili kuendelezwa na kuwa shule maalum kwa vigezo vilivyoainishwa:

3.2.1        Kia Sekondari – Shule Maalum ya Wavulana:
Ø  Inalo eneo la Ekari saba hivyo inaruhusu upanuzi wa shule;
Ø  Ipo karibu na Uwanja wa Kimataifa wa Ndege (KIA) ambao utakuwa kivutio kwa wanafunzi kupenda kujifunza sayansi;
Ø  Ni shule inayopokea wanafunzi wachache kila mwaka ambao ni rahisi kusomea katika shule tarajiwa ya Tambarare – Kijiji cha Mtakuja, Kata ya Kia.

3.2.2   Mukwasa Sekondari  -  Shule Maalum ya Wasichana:
Ø  Inalo eneo la Ekari 6.7 hivyo inaruhusu upanuzi wa shule;
Ø  Ipo katika kijiji cha Mungushi – kata ya Masama kusini, hivyo ni rahisi kufikika kutoka mji wa Bomang’ombe na kupata huduma muhimu za kijamii kwa urahisi;
Ø  Ni shule inayopokea wanafunzi wachache kila mwaka ambao ni rahisi kusomea katika shule jirani za Boma, Hai day na Lerai zilizopo katika Kata ya Hai Mjini.



3.3            Mikakati ya Kuimarisha Shule Mbili Maalum

Baada ya uteuzi wa shule mbili maalum kinachofuata ni kufanya tathmini na kutafuta namna bora na ya haraka ya kuziimarisha kwa miundombinu ya haraka ili zianze kupokea wanafunzi maalum wa kidato cha I, hapo Januari 2015.  Miundombinu inayohitajika kwa haraka kwa shule hizo ambayo haipo kwa sasa ni:
v  Mabweni yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kwa kuanzia kwa kila shule yenye thamani ya Tsh. 150,000,000.00 kila shule;
v  Maabara za masomo ya Sayansi – Multipurpose Laboratory yenye thamani ya Tsh. 45,000,000.00 kila shule;
v  Nyumba 2 – Mkuu wa Shule na Matron / Patron – kila shule, zenye thamani ya Tsh. 45,000,000.00 kila nyumba.

Katika kuhakikisha majengo haya yanajengwa kwa kila shule inahitajika jumla ya Tsh. 570,000,000.00.  Hivyo, mikakati iliyoamuliwa kutumika kwa ajili ya ujenzi na uimarishaji wa maabara ndio pia itumike katika zoezi hili la uimarishaji wa shule mbili maalum ambapo michango itokane na wananchi wote ndani ya Halmashauri na sio kwa kata husika tu.

4.0      MAPENDEKEZO YA UPATIKANAJI WA FEDHA ZA UJENZI

4.1      Makisio ya Awali ya Ujenzi wa Maabara na Shule Maalum

Katika kufanya makisio ya awali kwa kutumia viwango vya Mpango wa “MMES” imebainika kuwa jumla ya Tsh. 1,165,000,000.00 zinahitajika kukamilisha ujenzi wa maabara mpya na kuimarisha “Science rooms” zilizopo pamoja na kuongeza miundo mbinu muhimu kwa shule maalum sawa na mchanganuo ufuatao:
*      Ukamilishaji wa maabara ni Tsh. 685,000,000.00;
*      Ujenzi wa hosteli 4 katika shule mbili maalum ni Tsh. 300,000,000.00;
*      Ujenzi wa nyumba 4 za walimu katika shule mbili maalum ni Tsh. 180,000,000.00.

4.2      Njia za Kupata Fedha

Halmashauri ya Wilaya ya Hai, inakisiwa kuwa na jumla ya wakazi 210,533 – wanaume 102,457 na wanawake 108,076 – ambapo ni wakazi 96,355 (45.77%) – wanaume 45,876 na wanawake 50,479 – tu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa bidii (Kiambatisho “C”).  Wengine ni watoto na wazee wanaokisiwa kutokuwa na uwezo wa kuchangia maendeleo ya maeneo yao.  Katika kupata fedha za ujenzi yafuatayo yameamuliwa:

Ø  Halmashauri ya Wilaya imependekeza kila mwananchi mwenye uwezo wa kufanya kazi atakiwe kuchangia kwa wastani wa Tsh. 12,000/= na wakuu wa Idara na Waheshimiwa madiwani wachangie kila mmoja jumla ya Tsh. 50,000/= ambapo jumla ya Tsh.  1,165,895,500.00 zitakusanywa kutoka kwa wakazi 96,355 na kutimiza lengo la ujenzi wa miundombinu hitajika

Ø  Waheshimiwa madiwani, Maafisa Tarafa, watendaji wa Kata na Vijiji, walezi wa Kata na Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kila mmoja kwa nafasi yake waelekezwe kuchukua hatua za makusudi kukusanya michango, kusimamia ujenzi na kuhakikisha maabara zinajengwa shuleni mapema iwezekenavyo;

Ø  Halmashauri iunde na kuanzisha Mfuko wa Elimu wa Wilaya ambao utahusika zaidi kutafuta wafadhili na wahisani pamoja na kuratibu na kusimamia utekelezaji wa mapema ili kufanikisha ujenzi wa maabara na shule maalum kwa haraka iwezekanavyo ikiwa ni pamoja na kuweka msukumo wa pekee katika ukamilishaji wa shule tano (5) za Kidato cha V – VI sawa na malengo ya wananchi ya awali ndani ya Halmashauri.

4.3     Utaratibu wa Kukusanya Michango ya Wananchi
4.3.1        Ujenzi wa miundombinu ya shule umegawanyika katika vipengele vitatu ambavyo ni kama ifuatavyo:
Ø  Ujenzi wa maabara  = Tsh. 685,000,000.00
Ø  Ujenzi wa shule mbili maalum za Wilaya = Tsh. 570,000,000.00
4.3.2            Inashauriwa michango kutoka kwa kila mwananchi mwenye uwezo wa kufanya kazi achangie jumla ya Tsh. 15,000.00 ambayo itachangwa kwa utaratibu na mgawanyo ufuatao:
Maelezo
Kata Husika (maabara)
Halmashauri (Shule 2  maalum)
Halmashauri (Shule za Kidato  V - VI)
Jumla
Kiasi cha Mchango kwa Mwananchi Mmoja
7,000.00
5,000.00
3,000.00
15,000.00
Asilimia (%)
46.67
33.33
20.00
100

4.3.3            Katika bajeti ya mwaka 2014/2015, Halmashauri imetenga fedha kuwezesha ujenzi wa maabara 8 za sayansi na ununuzi wa vifaa na madawa vya maabara katika shule 8 za sekondari:-  KIA, Kikafu, Sawe, Kyuu, Tumona, Nkuu, Lukani na Lemira  = Tsh. Tshs. 513,540,000.00.
4.3.4            Katika bajeti ya mwaka 2014/2015, Halmashauri imetenga fedha kuwezesha ujenzi wa hosteli 2 za wanafunzi katika shule 2 za sekondari:- KIA – 2 (O-level) = 200,000,000.00.

5.0   HALI YA MADAWATI KATIKA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI
5.1   Shule za Msingi
Halmashauri ya wilaya ya Hai ina jumla ya shule 121 zikiwemo za binafsi 17 na 104 za serikali.  Katika shule za serikali, wapo jumla ya wanafunzi 14410 ambapo takwimu za madawati ni kama ifuatavyo kwa mwaka 2014:

MAHITAJI
YALIYOPO
UPUNGUFU
ASILIMIA
14,410
12,541
1,869
12.97%


5.1.1   Mikakati ya Kuondoa Upungufu

Katika kuhakikisha upungufu wa madawati katika Shule za Msingi unaondolewa, Halmashauri ya Wilaya imezielekeza Kamati za Shule kutekeleza yafuatayo:

*      kufanya ukarabati wa madawati 922 yaliyovunjika kwa kutumia kiasi cha 32% ya fedha za ukarabati kutoka katika “Capitation Grant”.
*      Kuhamasisha jamii, wadau wa Elimu hasa Taasisi /NGOs /CBOS katika kuchangia madawati halisi kwa kugharamia matengenezo ya madawati 947 mapya hasa kwa shule zenye upungufu mkubwa.

5.2   Shule za Sekondari
Katika shule za sekondari hakuna upungufu wowote wa madawati (viti na meza) ya wanafunzi kutokana na Sera ya Halmashauri iliyopo kwa mpango ufuatao:
*      Kuhakikisha wanafunzi wa Kidato cha I wanaleta kiti na meza kwa shule zinazopangiwa wanafunzi wengi kuliko idadi ya Kidato cha IV waliohitimu;
*      Wazazi kuchangia kiasi cha Tsh. 15,000/= kwa mwaka kwa kidato cha I kwa ajili ya kukarabati viti na meza vinavyokuwa vibovu au kuongeza idadi ndogo ya viti vinavyokuwa vinapungua.

6.0  CHANGAMOTO
Pamoja na juhudi za Halmashauri kuhimiza ujenzi wa maabara, shule mbili maalum za sekondari na matengenezo ya madawati kwa shule za msingi, bado changamoto zifuatazozinajitokeza mara kwa mara:
v  Mwamko hafifu kujitolea kuchangia maendeleo ya shule zao pamoja na ulipaji wa ada za uendeshaji wa shule;
v  Upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi na Hisabati kiasi cha walimu 69 kwa sasa – mahitaji ni walimu 177 lakini waliopo ni walimu 108;
v  Wanasiasa kutotaka kuhimiza michango ya ujenzi wa shule kwa hofu ya kupoteza kura kwa wananchi wao.

7.0      HITIMISHO
  
Katika kuboresha Elimu ya sekondari kufikia mapinduzi ya kisayansi katika elimu tunahitaji nguvu ya pamoja kama Halmashauri na Wilaya kufanikisha malengo ya Taifa katika Elimu ya Sekondari.

Ili mafanikio yapatikane ni lazima viongozi wa serikali na vyama vya siasa, wadau mbali mbali wa maendeleo pamoja na wananchi tushikamane licha ya changamoto ambazo zinajitokeza mara kwa mara na lazima tushinde.  Aidha, Halmashauri itaendelea kuzingatia Sheria, Taratibu na kanuni katika kusimamia utendaji kazi ili kufikia matarajio na malengo ya Taifa katika Elimu.

INAWEZEKANA KILA MMOJA ATIMIZE WAJIBU WAKE

Nawasilisha.

Humbe, M. O.
Mkurugenzi Mtendaji (W)
HAI

0 comments:

Post a Comment