MOSHI WAANZA MSAKO MKALI KWA WANAOUZA POMBE ZA KAZI

Posted by bomang'ombe On 11:44 No comments

Na Mwandishi Wetu,Moshi Halmashauri zote mbili katika wilaya ya Moshi zimeanza utekelezaji wa waraka namba moja wa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro unaohusu kudhibiti unywaji wa pombe usiozingatia sheria ya vileo nchini. Kaimu mkuu wa wilaya ya Moshi,Novatus Makunga amewaeleza waandishi wa habari mjini hapa kwamba halmashauri ya manispaa ya Moshi na halmashauri ya wilaya ya Moshi zote zilianza operesheni hiyo Desemba 15 ya mwezi uliopita. Ameeleza waraka huo uliagiza operesheni hiyo inayolenga kukomesha maduka ya kawaida kuuza pombe hususani viroba pamoja na baa kuuza vinywaji vikali saa za kazi ilitakiwa kuanza Desemba 15 mwaka jana. Makunga ameeleza kuwa operesheni hiyo ambayo itakuwa ya kudumu kama ile ya kudhibiti ukataji wa miti mkoani Kilimanjaro pia itazihusu pombe haramu ukiwemo ya gongo na zile feki zenye athali kubwa zaidi kwa binadamu. Amesema sheria ya muda ya kuuza pombe ipo wazi na ni sheria ambayo ilikuwepo tangu uongozi wa rais wa awamu ya kwanza ambapo kwa siku za mijini kwa katikati ya wiki ni kuanzia saa tisa mchana mpaka saa nne za usiku na kwa siku za mwisho wa wiki ni kuanzia saa sita mchana mpaka saa tano usiku. "Kadhalika ndani yake tunajumuisha mirungi pamoja na bangi ambavyo vimekuwa tatizo na janga kubwa katika jamii hususani kundi la vijana" alisisitiza. Amefafanua kwamba kwa upande wa manispaa ya Moshi imeanza kwa kuunda kamati maalumu ya kudhibiti unywaji wa pombe usiozingatia kanuni. Kamati hiyo pia inawaelimisha watumishi wote kuanzia ngazi ya mitaa kuhusu waraka huo pamoja na sheria nyingine za vileo,kutoa katangazo kwa jamii kuhusu kukemea unywaji wa pombe hovyo,kukagua na kuanisha maeneo yote yenye matatizo ya kupindukia ya ulevi. Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na kituo kikuu cha mabasi na baa zinazozunguka kituo hicho pamoja na mitaa yenye baa nyingi ambapo tayari kumekuwepo na misako ya kustukiza. Makunga amesema zoezi hilo linafanywa kwa ushirikiano kati ya maofisa wa manispaa na jeshi la polisi kwa uratibu wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya. Ameeleza kuwa mpaka mwishoni mwa wiki katika manispaa jumla ya madereva 15 walibainika kuwa wamelewa na kupigwa faini,lita nne za gongo pamoja na watuhumiwa kumi walikamatwa na pia kukamatwa kwa mirungi kilo 25 na watuhumiwa 4 pamoja na bangi kilo 50 na watuhumiwa 6. Kwa yale makosa ya kawaida yanayoangukia katika masuala ya leseni watuhumiwa wametozwa faini ya kati ya shilingi 40,000 na 50,000 na kwa makosa ya kijinai kesi zao zipo polisi tayari kufikishwa mahakamani. Makunga ameeleza kuwa kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Moshi hadi kufikia mwishoni mwa wiki misako mikali imefanyika eneo la Himo na Njiapanda ambapo zaidi ya maduka arobaini yalibainika kukiuka leseni za biashara. Aidha katika operesheni hiyo jumla ya kilo 20 za mirungi na watuhumiwa husika 3 walikamatwa na kufikishwa polisi na jumla ya kilo 81 za bangi na watuhumiwa 11 walikamatwa. Makunga ameeleza kuwa operesheni kabambe itaanza katika wiki inayoanzia Jumatatu ijayo baada ya kumalizika kwa shughuli za sikukuu za mwishoni mwa mwaka za Krismasi na mwaka mpya.

0 comments:

Post a Comment