WAKUU WA MIKOA NA WILAYA SIKU WALIPOWASILISHA MAONI YA RASIMU YA KATIBA

Posted by Arusha by day and by night On 05:42 No comments

Mwenyekiti wa wakuu wa mikoa ambaye ni mkuu wa mkoa wa Mbeya akitoa ufafanuzi wa maoni ya rasimu ya katiba kwa kundi la Ma-RC na Ma-DC katika ukumbi wa Habari maelezo
 
 
Picha na Magreth Kinabo – Maelezo.
Na Lydia Churi, MAELEZO -Agosti 28,2013


Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini wanapendekeza msingi mkuu wa kudai haki kwenye katiba mpya utanguliwe na wajibu ili watanzania wajenge utamaduni wa kuwajibika ambao utakuwa ni kichocheo cha maendeleo ya kasi na utii wa sheria kuanzia ngazi ya mtu binafsi,jamii na taasisi.    
    
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya jijini Dar es salaam leo, mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas kandoro alisema maoni yao kuhusu rasimu ya katiba ni juu ya muundo wa serikali, masuala ya kisheria, tunu na alama za taifa pamoja na wajibu na haki za raia.   
     
Alisema kuhusu muundo wa serikali Baraza lao la  Katiba linapendekeza serikali mbili kama ilivyo sasa yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kinyume na muundo uliopendekezwa na Rasimu ya Jamhuri ya Muungano ambao mfumo wake ni wa serikali tatu.

Alisema sababu za baraza hilo kupendekeza serikali mbili ni kutokana na kuona kuwa  kuwepo kwa serikali tatu kutakuwa na kila dalili ya rasilimali zinazotegemewa kuendesha serikali zote tatu zinazopendekezwa kutoka upande wa Tanzania Bara na hivyo kuuweka muungano katika hali tete ya kuweza kuhimili.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni nchi inaweza kuingia kwenye mgogoro mkubwa wa kikatiba endapo vyama tofauti vya siasa vitashinda uchaguzi kwenye kiti cha urais. Hata hivyo aliongeza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa kuwepo kwa serikali tatu kuna uwezekano wa kuvunjika kwa Muungano.

Kandoro alisema, wanapendekeza Katiba mpya itambue tunu ya amani na utulivu kuwa ni moja ya tunu na alama za taifa kwa kuwa amani na utulivu ndiyo msingi mkuu wa shughuli zote binafsi na za pamoja katika kufikia malengo yoyote kimaendeleo.

Alisema kuhusu masuala ya uraia yanayowagusa wananchi moja kwa moja na rasilimali zao wanashauri Katiba mpya itoe maelekezo ya wazi ili mtanzania awe ni mtu anayejipambanua  kwa sifa za wazi badala ya sifa zinazopendekezwa kwenye rasimu ya katiba ambazo mbeleni zinaweza kuleta utata katika maeneo mbalimbali.

Alisema baraza hilo pia linapendekeza kuongezwa kwa kipengele cha kudumisha na kuhakikisha rasilimali za nchi zinamilikiwa na watanzania. Baraza baraza hilo linaafiki masuala ya mgombea huru pamoja na mawaziri kutotokana na wabunge.

Kuhusu kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kandoro alisema sharti la kuzaliwa la mgombea wa kiti hicho kwenye katiba mpya lisomeke kuwa awe ni raia wa kuzaliwa kwa baba na mama.

Aidha, mkuu huyo wa mkoa amewataka watanzania kuipitia rasimu ya katiba kwa makini na kutoa maoni juu ya mambo mbalimbali yaliyomo kwenye rasimu hiyo badala ya kujadili zaidi suala la nafasi ya urais na muundo wa serikali peke yake. 

Alisema kama rais Jakaya Kikwete alivyowasisitiza watanzania kuipokea katiba mpya wao pia watakuwa tayari kuikubali na kuipokea katiba mpya hata kama waliyoyapendekeza hayataingia kwenye katiba hiyo

0 comments:

Post a Comment