Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mheshimiwa Leonidas Gama
Kwa Mujibu wa Rasimu ya Katiba wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Sura ya sita na Ibara zake inazungumzia kuwapo kwa muundo wa
shirikisho wa serikali tatu.Serikali ya Muungano, serikali ya Tanzania bara na
Serikai ya zanzibar na kwamba kudumu kwa Muungano pamoja na sababu nyingine
ni dhamira ya Watanzania wote.
Ni kweli Muungano ni dhamira ya dhati ya wanaoungana na
kwa Muungano wetu ni dhamira ya Watanzania wote, dhamira ya dhati ya
kuudumisha muungano ni ile ambayo inakubalika na inaendana na Matakwa ya
walio wengi.
|
Kwa mazingira ya nchi yetu na mazingira ya kibinadamu, sio
rahisi katika Taifa kama hili lenye watu zaidi ya milioni arobaini,
tukawa na dhamira moja, tutajiridhisha kinadharia tu kuwa Muungano utadumu
kwa vile tuna dhamira nao, huku ni kujidanganya. Ni dhahiri kuwa ikitokea
katika mfumo huu wa serikali tatu, tukapata kiongozi mkuu, ama chama, ama
chombo chenye mamlaka ya kutunga sheria, ama kundi la watu ambalo dhamira yao
ni tofauti na dhamira ya wengi.
Ni wazi kuwa pamoja na dhamira nzuri ya walio wengi wa
kudumisha Muungano wa sasa, Muungano utavunjika kwa matakwa ya mamlaka
iliyopo. Kwa maoni yangu Dhamira ya Watanzania katika kudumisha Muungano ni
sehemu tu ya kuimarisha na sio suluhisho la kudumu kwa Muungano.
Muundo madhubuti unaozuia fursa ya kuvunja Muungano ndio
suluhisho sahihi na la kudumu kwa Muungano. Ni vyema Watanzania
tusisahau yale ya mwaka 1977, tulikuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, wote
wana Afrika Mashariki tuliipenda Jumuiya yetu, tulikuwa na dhamira ya dhati
ya kuidumisha.
Lakini alitokea mtu mmoja tu kwa matakwa yake, na akili
zake alizoziona zinafaa alisababisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvunjika
sembuse Muungano wa Serikali tatu?
Waasisi wa Taifa letu, Hayati Abeid Amani wa Zanzibar na
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika, karume walipoanzisha
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hawakukurupuka, walikuwa na sababu za
msingi za kuunganisha nchi mbili hizi.
Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na Undugu wa damu
uliopo kati ya Wananchi wa Zanzibar na Tanganyika na pili ni sababu za
kiulinzi na usalama kwa nchi hizi wa mali, rasilimali na watu wake, ninaamini
kuwa, sababu hizi bado ni hai hadi sasa na ni sababu muhimu kwa
mustakabali wa Taifa letu.
Watanzania hivi sasa kupitia mabaraza mbalimbali
wanaendelea kutoa na kukusanya maoni juu ya katiba. wapo wanaopita huku na
huko na wale wanaotumia njia mbalimbali za kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya
Katiba na hasa eneo hili la muundo wa serikali tatu.
Ni uhuru wa kila mtu kutoa maoni yake, lakini kuna haja ya
Watanzania kuwa na tahadhari sana, wapo wanaojua fika kuwa kuwepo kwa
serikali tatu, zenye Marais watatu katika nchi yenye mamlaka tatu, ni
kuuvunja Muungano.
Hivyo wapo wanaoshabikia serikali tatu, si kwa kuimarisha
Muungano ila wanajua kuwa ni kuuvunja Muungano. Wanachelea kuonyesha dhamira
yao ya kuuvunja Muungano bali wanashabikia Serikali tatu kwa kujua dhamira
yao itatimia.Watanzania tutafakari, tuchukue Hatua
Pamoja na Sababu nyingine nyingi unazoweza kuzichambua juu
ya kudumu au kutokudumu kwa Muungano wa Serikali tatu, nimeona ni vyema
nipitie maeneo ambayo binafsi nimeona yanaweza kuchochea kuunjwa kwa Muungano
wa serikali tatu.
Wengine wanajadili hoja ya gharama kubwa za kuendesha
serikali tatu, kwangu hili si hoja, naamini jambo lolote la kheri linahitaji
gharama na kama gharama zinaweza kuhimilika, hilo si tatizo.Maeneo yanayoweza
kuvunja muungano ni pamoja na:
(i)Uwezo uliosawa ki-uwiano katika kuchangia uendeshaji wa
Muungano
katika ibara ya 215 ya Rasimu, inazungumzia vyanzo vya
mapato ya serikali ya Jamhuri ya Muungano, na moja kati yake ni "mchango
kutoka kwa washirika wa Muungano" maana yake ni mchango toka serikali ya
Zanzibar na kutoka ya Tanzania bara.
Ni dhahiri muundo na mfumo wa uendeshaji wa serikali ya
Muungano kiasi kikubwa utategemea mchango huu ambao unategemea uchumi wa
serikali mbili zinazounda Muungano, katika mazingira halisi ya Tanzania kwa
kuzingatia rasilimali na mali zilizopo katika maeneo ya Muungano yaani Tanzania
Bara na Zanzibar ni dhahiri hayatawezesha mchango ulio sawa ki-uwiano katika
kuendesha serikali ya Muungano, hii itaifanya Serikali yenye mazingira mazuri
ya mali na rasilimali, kulazimika kuiendesha/kuichangia Serikali ya Jamhuri
ya Muungano na nyingine kushindwa kuchangia katika hali yoyote ile, mgongano
wa kiuchumi na kimaslahi hautaepukika.
Lakini pia katika mazingira ya umoja na mshikamano uliopo
sasa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo
ushirikiano katika uendeshaji wa shughuli za kiserikali ni ule usioepukika,
(Gharama za uendeshaji na huduma katika serikali kwa mfano- Umeme , Mafuta
n.k.)
Hali hiyo katika serikali tatu, haitapata nafasi, serikali
itakayochangia zaidi tofauti na nyingine haitakubali hali hiyo. kwa maana ya
kiuchumi, pia upo uwezekano wa serikali itakayoshindwa kujiendesha au hata
kuchangia, kukopa nje katika mazingira ya kupoteza uhuru wake wa kiuchumi na
kiusalama.
Tukumbuke kuwa hadi sasa bado waptu nje ya nchi
wanaoitazama Zanzibar kisiwa chetu kizuri kama eneo lao, na bado wanandoto
kuwa siku moja watarudi Zanzibar kiutawala.Jee iwapo Zanzibar itashindwa
kuchangia katika serikali ya Muungano na kujiendesha kiuchumi ni nini
kitatokea?
Ni lazima tukubali Watanzania kuwa uchumi wa nchi hizi
unatofautiana sana na kuishi kwetu katika Muungano ni kule kwa kushirikiana
kindugu kunakotokana pia na mfumo uliopo wa Muungano, vinginevyo kwa muundo
wa serikali tatu, zenye Marais watatu, hili linalofanyika sasa halina nafasizi,
ni wazi kuwa nafasi ya kudumu kwa Muungano itakuwa matatani.
(ii) Mgawanyo wa madaraka na mfumo wa kiutawala
Kwa mujibu wa Rasimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kutakuwa na Marais watatu na serikali tatu na kwa mujibu wa madaraka
na mamlaka, kila Rais atakuwa na madaraka katika eneo lake la utawala.
Katika mfumo wa miliki za mali na rasilimali na utawala wa
mali na rasilimali za nchi, kwa sehemu kubwa utakuwa katika mamlaka za
serikali ya Zanzibar kwa eneo la Zanzibar na Tanzania bara kwa yaliyo chini
ya Tanzania bara.
Hii ni pamoja na utawala wa serikali, serikali za mitaa,
tawala za mikoa na uteuzi wa mamlaka za utendaji, Ardhi, Maji, Barabara,
Huduma za kijamii ikiwemo Elimu, Afya n.k.
Kiutawala Rais wa Jamhuri ya Muungano hatakuwa na eneo la
utawala kirasilimali hasa rasilimali watu, Rais wa Muungano hatakuwa na
mamlaka na madaraka za kiutendaji, rasilimali na huduma za kijamii na za
maendeleo, mamlaka za kuagiza wala kukemea.
Katika hali hii utendaji kazi wa Rais wa Muungano ambaye
ndiye Kiongozi Mkuu, hautakuwa wenye mamlaka na madaraka. Uwepo wa mgongano
wa kimadaraka kati ya Jamhuri ya Muungano na serikali ya Zanzibar na ile ya
Tanzania bara hautazuilika. Na ni ukweli Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa
Boya, ataelea hewani.
(iii) Mfumo wa utawala na Vyama vingi vya siasa
Kwa mujibu wa sura ya kwanza ya Ibara ya 1 (2) ya Rasimu
ya Katiba, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni shirikisho la kidemokrasia
linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Kwa mtazamo wangu; katika mfumo wa kidemokrasia
unaozingatia vyama vingi vya siasa, ni dhahiri kuwa utawala na mamlaka za
utawala zinaweza kuwa katika matokeo ya mchanganyiko mkubwa wa Vyama
mbalimbali vya kisiasa, matokeo ya chaguzi za Rais, wabunge na Madiwani
zinaweza kutoa sura tofauti na katika maeneo tofauti.
Ni ukweli kuwa kila chama cha siasa, kina mfumo wake na
malengo yake, kisiasa tunaamini nchi ni moja, na wote tunajenga nyumba moja
kwa hiyo tofauti zetu za kisasa zisivuruge umoja na mshikamano wetu. Kwa
nadharai ya kisiasa, hii ni sahihi, lakini kihalisia ni dhana isiyotakiwa
kuiamini.
Upo uwezekano wa chaguzi katika serikali tatu, zikapata
vyama vinavyoongoza serikali kwa tofauti kwa kila eneo la utawala: kwa mfano
serikali ya Jamhuri ya Muungano ikaongozwa na chama kingine, Serikali ya
Zanzibar ikaongozwa na chama kingine na ile ya Tanzanzia Bara inkaongozwa pia
na chama kingine.
|
Kwa
vyovyote vile mamlaka na madaraka yatawataka Marais wa Bara na yule wa Zanzibar
kutii mamlaka ya Rais wa Muungano. Ni rahisi sana kusema hakuna tatizo lolote,
wataongozwa na Katiba lakini yeyote anayejua mwenendo wa siasa za Tanzania hivi
sasa na matarajio za siasa za baadae zinazoendelea hapa nchini, kwa tofauti ya
sera, itikadi na mitazamo ya kimaslahi katika vyama vyetu na jamii kwa ujumla.
Kwa
mtazamo wa yeyote yule ni kuwa Muungano huu wa serikali tatu, wenye Marais
watatu ni ndoto kuamini kuwa utadumu katika mazingira ya utawala wa vyama
tofauti katika serikali zilizopo.
Tukumbuke
Historia ya Muungano iliyoundwa kwa utaratibu unaofanana na huu ambao umeishia
kusambaratika kama vile Muungano wa iliyokuwa Yugoslavia na Usavieti. Katika
Yugoslavia, jimbo la Albania, ndilo lilikuwa la kwanza kutaka kujitenga na
hatimaye kulitumbukiza Taifa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe huku na
majimbo mengine kama Serbia na Montenegro yakidai kujitawala; hatima na matokeo
ya Muungano huo ni Kuvunjika kwa Muungano wao.
Zipo
nchi nyingi zimesambaratika kutokana na mifarakano midogo midogo ya kijamii:
kumbuka Ethiopia, Eritrea, Somalia, Sudani na Sudani ya Kusini n.k
"Mimi
bado naamini kuwa suluhisho la kero la Muungano siyo kuwa na serikali tatu,
bado tunao uwezo na nafasi kubwa ya mjadala zaidi.Tujiulize ni nchi gani
duniani yenye Marais wa watatu, wenye serikali tatu na wakakaa katika mfumo huu
wa Muungano wakafanikiwa?
tujifunze
kutoka kwa wenzetu walioungana duniani, Marekani imeundwa na majimbo zaidi ya
52, lakini pamoja na majimbo hayo kuwa na nguvu na rasilimali zote, bado Rais
mwenye Nguvu ni mmoja tu.
Marekani
haijagawa mamlaka, madaraka, usimazi, utawala na maamuzi kwa mtu zaidi ya mmoja
na ndio maana Taifa la Marekani linaendelea kuwa imara sio ndani tu bali hata
nje ya mipaka yake.
Watanzania
wa Bara na Visiwani, kama tunadhamiria kweli kujenga umoja wa kitaifa kwa mfumo
wa Serikali tatu tungekuwa na Serikali zenye muundo huu; Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania yenye Rais aliyechaguliwa na Watanzania wote.
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Waziri Mkuu mtendaji aliyechaguliwa na Bunge la
Jamhuri Serikali ya Tanzania Bara aliyechaguliwa na Bunge la Jamhuri ya
Muungano.
Hili
ndilo suluhisho pekee kwa wale wanaotaka Serikali tatu, lakini nina hakika kwa
sababu za tulio wengi kutawaliwa na homa ya madaraka, wazo hili wengi
watalipuuzia bila kujali kuwa ndilo suluhisho.
Tujiulize
ni kweli tunautaka Muungano au tunasema tunaimarisha Muungano kumbe dhamira
zetu zinataka tuone Muungano unakufa kwa vile eti kwa nini Zanzibar wana
bendera yao, wana wimbo wao wa Taifa, wana madai yao kila kukicha.
Watanzania
wenzangu, Muungano unaondoka, chozi la Baba wa Taifa litatushukia. Kuna tafsiri
fulani nimesikia zikitolewa na wale wanaotetea muundo wa serikali tatu, Jaji
Warioba na kundi lake katika tafsiri zao nimesikia wakimnukuu Baba wa Taifa
kupendekeza serikali tatu.
Tuache
kutafsiri na kupindisha maneno ya Baba wa Taifa kwa kile tunachokitaka sisi,
maana wapo wanaotumia maandishi mbalimbali ya Baba wa Taifa, kumpandikizia
tafsiri ya kutaka serikali tatu kwa matakwa yao.
Baba
wa Taifa amefariki akiamini na akiwa na msimamo mmoja tu “Muungano wa Serikali
mbili kuelekea serikali moja”. Mwanamapinduzi Mzee Abeid Amani Karume amefariki
akiamini juu ya Tanzania yenye Muungano wa Serikali moja.
Mungu
Ibariki Muungano wetu. Mungu ibariki Tanzania.
Makala
hii imeandaliwa na Mwalimu Leonidas T. Gama
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro.
haya
ni Mawazo binafsi na Mapendekezo yangu!
Imetolewa Agosti 28,2013