VIJIJI VITANO WILAYANI HAI KUPATA MAJI IFIKAPO SEPTEMBA 30 MWAKA HUU

Posted by Arusha by day and by night On 04:45 No comments

m
Moja ya tanki linalopeleka maji katika kijiji cha Mbatakero

Na Mwandishi Wetu Hai

Wilaya ya Hai itakamilisha ufikishaji wa maji safi na salama katika vijiji vitano kupitia mkakati wa sasa wa serikali wa Mfumo mpya unaolenga kuleta mapinduzi ya kijamii nchini wa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo unaojulikana kama matokeo makubwa sasa yaani “Big Results Now” ifikapo Septemba 30 mwaka huu.

Vijiji hivyo vitano kati ya kumi ambavyo kwa kila Halmashauri nchini itahakikisha vinaingizwa katika mpango wa kupata huduma ya maji safi na salama ni Mbatakero,Ngosero,Kwasadala,Kimashuku na Kwatito ambavyo vitaunganishwa na maji safi na salama ya Bomba kutokea katika Skimu ya Lyamungo-Umbwe.

Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga akizungumza katika mikutano mbalimbali ya vijiji vya Ngosero na Mijongweni mwishoni mwa wiki ameeleza kuwa maji hayo yatafika kwa umbali wa kilometa 22.73 na utekelezaji wa kazi umefikia asilimia 85.

Ameanisha kazi ambazo tayari zimeshakamilika ni pamoja na ujenzi wa chemba ya kuchukulia maji,ujenzi wa kivuko kutoka mto kikafu,ujenzi wa matanki mawili ya lita za ujazo 50,000 kila moja,ujenzi wa vilula 20,kuchimba mtalo kilometa 21,kulaza na kufukia mambomba kilometa 20

Amewahakishia wananchi wa vitongoji viwili ambavyo viliachwa katika mradi huo vya Landi na Jitengene katika kijiji cha Ngosero nao watapata maji ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba

Amefafanua kuwa katika mpango huo kijiji cha Kimashuku kitahusu vitongoji vya Kinyalu na Kiangaa,Kijiji cha Kwasadala kitongoji cha Faraja na kijiji cha Kwatito ni kitongoji Kasendero

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaweza kupatikana kwa huduma ya maji kwa wakazi zaidi ya 3,443 katika umbali uziozidi mita 400.

Makunga amesema baada ya kukamilika kwa awamu hiyo ya kwanza,serikali wilayani humo itaanza mara moja utekelezaji wa awamu ya pili ya upelekaji wa maji katika vijiji vitano ambayo inatakiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni mwakani.

Ametaja vijiji vitakavyohusika na awamu ya pili kuwa ni pamoja na Sanya Stesheni,Chemka,Mtakuja na Tindigani pamoja na mji wa Bomang’ombe kupitia Skimu ya maji ya Losaa-Kia

“Hivi vijiji vya awamu ya pili vilikuwa na tatizo kubwa sana la maji kwa muda mrefu kutokana na kukosa kabisa chanzo chochote chenye maji safi na salama kutokana na maji ya maeneo hayo kuwa na kiasi kikubwa cha madini ya floride ambayo yamekuwa na athali kubwa kiafya kwa watumiaji na hasa watoto wadogo,”amefafanua

Akifafanua kuhusiana na mji wa Bomang’ombe,Makunga ameeeza kuwa hivi sasa unakabiliwa na uhaba wa maji kutokana na ongezeko kubwa na la kazi la watu kutokana na wenyeji wengi wa mji ya Moshi,Arusha,Mererani na Sanya juu kupenda kuweka makazi yao katika mji huo.

Ameeleza kuwa mji wa Bomang’ombe unaopata maji kutoka skimu ya Uroki-Bomang’ombe ilisanifiwa kwa kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wapatao 10,000.

Kutokana na ongezeko la wakazi wa mji wa Bomang’ombe na kufikia 34,000 kwa sasa,huduma ya maji safi na salama katika mji huo haikidhi matumizi kwa wakazi kwa siku.

Maeneo yenye upungufu wa maji katika mji huo ni Bomani juu na hususani hospitali ya wilaya ambayo kwa kipindi cha kiangazi inapata huduma ya maji wakati wa usiku tu.

0 comments:

Post a Comment