Moja ya tanki linalopeleka maji katika kijiji cha Mbatakero
Na Mwandishi Wetu Hai
Wilaya ya Hai itakamilisha
ufikishaji wa maji safi na salama katika vijiji vitano kupitia mkakati wa sasa
wa serikali wa Mfumo mpya unaolenga kuleta mapinduzi ya kijamii nchini wa
usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo unaojulikana kama matokeo
makubwa sasa yaani “Big Results Now” ifikapo Septemba 30 mwaka huu.
Vijiji hivyo vitano kati ya kumi
ambavyo kwa kila Halmashauri nchini itahakikisha vinaingizwa katika mpango wa
kupata huduma ya maji safi na salama ni Mbatakero,Ngosero,Kwasadala,Kimashuku
na Kwatito ambavyo vitaunganishwa na maji safi na salama ya Bomba kutokea
katika Skimu ya Lyamungo-Umbwe.
Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus
Makunga akizungumza katika mikutano mbalimbali ya vijiji vya Ngosero na
Mijongweni mwishoni mwa wiki ameeleza kuwa maji hayo yatafika kwa umbali wa
kilometa 22.73 na utekelezaji wa kazi umefikia asilimia 85.
Ameanisha kazi ambazo tayari
zimeshakamilika ni pamoja na ujenzi wa chemba ya kuchukulia maji,ujenzi wa
kivuko kutoka mto kikafu,ujenzi wa matanki mawili ya lita za ujazo 50,000 kila
moja,ujenzi wa vilula 20,kuchimba mtalo kilometa 21,kulaza na kufukia mambomba
kilometa 20
Amewahakishia wananchi wa vitongoji
viwili ambavyo viliachwa katika mradi huo vya Landi na Jitengene katika kijiji
cha Ngosero nao watapata maji ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba
Amefafanua kuwa katika mpango huo
kijiji cha Kimashuku kitahusu vitongoji vya Kinyalu na Kiangaa,Kijiji cha
Kwasadala kitongoji cha Faraja na kijiji cha Kwatito ni kitongoji Kasendero
Amesema kukamilika kwa mradi huo
kutaweza kupatikana kwa huduma ya maji kwa wakazi zaidi ya 3,443 katika umbali
uziozidi mita 400.
Makunga amesema baada ya kukamilika
kwa awamu hiyo ya kwanza,serikali wilayani humo itaanza mara moja utekelezaji
wa awamu ya pili ya upelekaji wa maji katika vijiji vitano ambayo inatakiwa
kukamilika ifikapo mwezi Juni mwakani.
Ametaja vijiji vitakavyohusika na
awamu ya pili kuwa ni pamoja na Sanya Stesheni,Chemka,Mtakuja na Tindigani
pamoja na mji wa Bomang’ombe kupitia Skimu ya maji ya Losaa-Kia
“Hivi vijiji vya awamu ya pili
vilikuwa na tatizo kubwa sana la maji kwa muda mrefu kutokana na kukosa kabisa
chanzo chochote chenye maji safi na salama kutokana na maji ya maeneo hayo kuwa
na kiasi kikubwa cha madini ya floride ambayo yamekuwa na athali kubwa kiafya
kwa watumiaji na hasa watoto wadogo,”amefafanua
Akifafanua kuhusiana na mji wa
Bomang’ombe,Makunga ameeeza kuwa hivi sasa unakabiliwa na uhaba wa maji
kutokana na ongezeko kubwa na la kazi la watu kutokana na wenyeji wengi wa mji
ya Moshi,Arusha,Mererani na Sanya juu kupenda kuweka makazi yao katika mji huo.
Ameeleza kuwa mji wa Bomang’ombe
unaopata maji kutoka skimu ya Uroki-Bomang’ombe ilisanifiwa kwa kutoa huduma ya
maji safi na salama kwa wakazi wapatao 10,000.
Kutokana na ongezeko la wakazi wa
mji wa Bomang’ombe na kufikia 34,000 kwa sasa,huduma ya maji safi na salama
katika mji huo haikidhi matumizi kwa wakazi kwa siku.
Maeneo yenye upungufu wa maji
katika mji huo ni Bomani juu na hususani hospitali ya wilaya ambayo kwa kipindi
cha kiangazi inapata huduma ya maji wakati wa usiku tu.