RAIS KIKWETE AAGIZA KUHARAKISHWA KWA UJENZI BARABARA YA KWASADALA-MASAMA

Posted by MK On 21:56 No comments

 Rais Jakaya Kikwete akiwasili katika kijiji cha Roo kwa ajili ya uzinduzi wa barabara ya Kwasadala-Masama wilayani Hai
 Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Kilimanjaro pamoja na wilaya ya Hai pamoja na wabunge mara baada ya uzinduzi wa barabara ya Kwasadala-Masama
 Rais Jakaya Kikwete akizindua moja ya mtambo utakaotumika katika kazi ya ujenzi wa barabara hiyo
Rais Jakaya Kikwete akizindua rasmi ujenzi wa barabara ya Kwasadala-Masama(Picha zote kwa hisani ya Ikulu)


Na Mwandishi wetu,Hai

Rais Jakaya Kikwete ameagiza ujenzi wa Barabara ya Kwasadala hadi Masama,wilayani Hai mkoani Kilimanjaro uanze kwa kasi kwa kurekebishwa dosari zote zilizojitokeza.

Rais Kikwete ametoa agizo hilo katika Kijiji cha Roo kilichopo katika kata ya Masama Mashariki, wilayani humo wakati anaweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo.

Rais Kikwete alisema ujenzi wa barabara hiyo aliamua yeye ijengwe kwa sababu katika wilaya nzima ya Hai, eneo la Masama ndilo pekee ambalo halikuwa na barabara ya lami.

“Kazi imeanza, lakini kwa bahati mbaya imechelewa sana, sitaki kuingia kwenye sababu za kuchelewa na kwamba nilipoanza ziara niliarifiwa hakuna kinachoendelea,” alisema.

Alisema kuwa licha ya kudokezwa hivyo,aliamua lazima aweke jiwe la msingi na anaamini dosari zilizojitokeza zitamalizwa na ujenzi uanze kwa kasi kama ilivyotarajiwa.

Aidha Rais Kikwete aliagiza wizara ya ujenzi kuhakikisha barabara hiyo inaunganishwa kwa kiwango cha lami na barabara inayokwenda Machame kwa upande wa mashariki pamoja na Barabara ya Sanya juu inayounganisha kati ya Bomang’ombe na wilaya ya Siha kwa upande wa magharibi.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo,waziri wa Ujenzi  Dk John Magufuli aliipa Kampuni ya Atlantic Market Ltd inayojenga barabara hiyo siku 60 za kuwasilisha kwake mpango wa jinsi itakavyokamilisha ujenzi wa barabara hiyo

Dk Magufuli aliiagiza vyombo vyote vinavyowasimamia makandarasi pamoja na wahandisi ikiwemo bodi ya wakandarasi nchini (CRB) kuichukulia hatua kampuni hiyo iwapo ndani ya siku hizo 60, itakuwa haijawasilisha mpango wa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ya kilomita 12.5.

Waziri huyo alifafanua kwamba ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh5.4 bilioni ulianza Mei 2010 na ulitakiwa uwe umekamilika na kukabidhiwa mwezi Mei mwaka jana.

Dk Magufuli ameeleza kuwa mkandarasi wa kampuni hiyo ambayo mkurugenzi mkuu wake ni Gabriel Mrema aliyekuwapo wakati wa uzinduzi huo ameshalipwa Sh1.6 bilioni na ameshatengeneza certificate (vyeti) saba na zote amelipwa, kwa hiyo haidai serikali kwa kazi aliyofanya.

 ”Nina kuahidi mheshimiwa Rais mara utakapoondoka Mimi,Mkandarasi na mtaalamu mshauri tukakomeshana na kamwe sitakubali kutimuliwa kazi kwa ajili ya uzembe wake kabla mimi hujanifukuza,yeye nitakuwa nimeshamtema,”alisisitiza waziri Magufuli

Huku akishangiliwa na wananchi, Dk Magufuli alisema yeye hayupo tayari kufukuzwa kazi kwa sababu ya kilomita 12.5, hivyo anataka wahusika wawe wametangulia kufukuzwa.

Waziri Magufuli alisema baada ya Rais kuondoka eneo hilo, bodi ya wakandarasi na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads), watakaa na mkandarasi kujua watakavyoshughulika naye.

“Nakupa siku 60 uje na mpango wa kukamilisha barabara hii, usipofanya hivyo bodi ya makandarasi ianze kukushughulikia ikiwezekana ufutwe kabisa ukandarasi ili ukavue samaki,” alisema.

Alisema haiwezekani mkataba unasainiwa, mkandarasi anafanya kazi hovyohovyo kwa kutengeneza kilomita nne za lami kwa miaka mwili, huku akihoji kama angepewa kilomita 100 ingekuwaje.

Dk Magufuli alisema huo ni mfano wa makandarasi wazalendo ambao hivi karibuni walilalamika mbele ya Rais Kikwete kuwa, wananyimwa kazi na serikali na kupendelea kampuni za nje.

Alitumia fursa hiyo kumweleza Mbunge wa Hai,Mheshimiwa Freeman Mbowe aliyekuwa ameketi jukwaa kuu kuwa, angalau sasa amefahamu mkandarasi ni tatizo katika kukamilisha barabara hiyo kwa wakati.

Aidha Dk Magufuli alimpongeza Mheshimiwa Mbowe kwa kutambua na kukiri hadharani kazi kubwa ya kuboresha huduma za kijamii inayofanywa na Rais Kikwete na kumtaka ajitahidi kuwaelimisha viongozi wenzake wa vyama vya upinzani.

“Mheshimiwa Mbowe leo umeongea maneno ya utukufu ambayo yanakubalika hata kwa mwenyezi Mungu,wewe kama kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na mwenyekiti wa Chadema ni vyema sasa ukawaelimisha na wenzako wachache wanaojifanya hawaoni kazi zinazofanyika,”alifafanua Dk Magufuli.

Kwa upande wake Mheshimiwa Freeman Mbowe alimpongeza Rais Kikwete kwa uchapaji kazi ambao umewezesha nchi kuwa na miondombinu bora ikiwemo ya barabara.

“Mimi ninasafiri karibu nchi nzima kwa njia mbalimbali yaani ndege na magari,jamani mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni,Rais Kikwete anastahili kupewa sifa kwa kazi kubwa anayoifanya.

Mbunge huyo wa Hai pia alitumia firsha hiyo kutoa ombi kwa Rais Kikwete la kuongeza kipande cha urefu wa barabara hiyo kwa kilometa nne ili kiweze kuunganishwa na barabara nyingine ya Machame.

Kadhalika Mheshimiwa Mbowe alimuomba Rais kuingilia kati madai ya fidia ya wananchi wapatao 390 waliokuwa wanamiliki ardhi katika mji wa Bomang’ombe ambao waliamishwa kwa ajili nya kujengwa kwa mji huo ambao ni makao makuu ya wilaya ya Hai.

0 comments:

Post a Comment