BIBI WA KIJERUMANI AIPIGA JEKI SHULE YA MSINGI CHEMKA

Posted by MK On 10:07 No comments

 Bibi Elisabeth Dorr akipokeza zawadi ya kitenge na mkeka kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Chemka
 Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga mara baada ya kupokea majengo ya shule ya msingi ya Chemka yaliyofadhiliwa na Bibi Elisabeth Dorr.Wengine katika picha ni mkurugenzi wa Shirika la AKO-Moshi, Klaus Peter Kiefe(wa saba kulia),mwalimu kutoka Ujerumani Barbara(wa sita kutoka kulia) na Oscar wa tatu kulia.
 Mgeni rasmi katika hafla ya kupokea majengo ya shule ya msingi ya Chemka Novatus Makunga akiwa na washirika wa maendeleo kutoka Ujerumani wakiongozwa na Bibi Elisabeth Dorr
 Sehemu ya jengo la bwalo la chakula la shule ya msingi ya Chemka lililojengwa na bibi Elisabeth Dorr
 Mabenchi na meza katika bwalo la chakula shule ya msingi ya Chemka
 Bibi Elisabeth Dorr akikumbatiana na baadhi ya akinamama wa kijiji cha Chemka baada ya kufurahishwa na zawadi mbalimbali


Na Richard Mwangulube,Hai

Shule ya Msingi ya Chemka iliyopo nje kidogo wa mji wa Bomang’ombe wilayani Hai,mkoani Kilimanjaro imepokea majengo yaliyojengwa na Bibi Kizee wa Kijerumani Elisabeth Dorr(89) kupitia shirika la Ako lililoko mjini Moshi.

Shule hiyo iliyopo katika kijiji cha Chemka ilipata ufadhili huo mwaka 2008 kupitia kanisa katoliki parokia ya Chekereni kupitia shirika la AKO-Moshi

Majengo hayo ni pamoja na madarasa matatu,nyumba mbili za walimu,bwalo la chakula,stoo na ofisi ya shule pamoja na kugharamia uunganishaji wa umeme na kuvuta maji ya bomba ambapo Bibi Dorr alitoa jumla ya Euro 50,000 ambazo ni sawa na shilingi 93,554,698.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo,David Mosha ameeleza kuwa Bibi huyo wa Kijerumani pia katika fedha hizo alitoa madawati 66,meza 4,viti 4,makabati 7 ya ukutani,sufuria mbili kubwa,beta stoves 2,meza na benchi 15 kwa ajili ya matumizi ya bwalo

Mosha ameeleza kuwa awali Bibi huyo alijenga darasa moja mwaka 2008 na baadaye mwaka uliofuata alimtuma mwenyekiti wa Shirika la AKO-Tanzania,Klaus Boehme na kufurahishwa na usimamizi wa miradi hiyo shuleni hapo.

Aidha Mosha ameeleza kuwa mkuu wa AKO-Moshi alitoa michoro ya ramani tatu za ukutani na michoro sita ya somo la sayansi na kibao cha shule vikigharimu shilingi 800,000/=

Ameeleza kuboreshwa kwa shule hiyo kumeinua kiwango cha ufaulo ambapo mwaka 2008 asilimia 78 waliweza kufaulu,mwaka 2009 asilimia 79,mwaka 2010 asilimia 69 na mwaka jana asilimia 66 huku akieleza kwa mwaka huu wanatarajiwa ufaulu kuwa asilimia 100

Akipokea rasmi miradi hiyo,Mkuu wa wilaya ya Hai Novatus Makunga amewataka wakazi wa kijiji cha Chemka kuyatunza majengo hayo kwa nguvu zao zote na pia kuhakikisha wanaingia katika kampeni ya kupanda miti kutokana na eneo hilo kunyemelewa na jangwa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mifugo

Aidha Makunga amewataka kutumia fursa ya vyumba bora na vizuri pamoja na umeme kuchangia ununuzi wa kompyuta kwa ajili ya kuanzisha darasa la kompyuta pamoja na kurahisisha kazi za utawala.

Aliahidi kuchangia kompyuta moja kwa ajili ya kuanzia na kuongeza kuwa siyo kwamba kukiamilika kwa majengo hayo kutaifanya shule hiyo kufanana na shule za mjini lakini pia kutawaingia katika mazingira ya kisasa ya teknolojia zinazotumika katika maeneo ya mjini





0 comments:

Post a Comment