MWENGE WA UHURU KUINGIA WILAYANI HAI KESHO

Posted by MK On 02:08 No comments


Na Richard Mwangulube,Bomang'ombe
 
 Kampuni ya nguo ya A to Z ya Arusha,imetoa msaada wa fulana mia tano na hamsini kwa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ajili ya mbio za mwenge wa Uhuru mwaka huu.

Mkurugenzi  mkuu wa A to Z,Bwana Anuj Shah amekabidhi rasmi fulana hizo kwa mkuu wa wilaya ya Hai,Bwana Novatus Makunga.

Shah ameeleza kuwa kwa kutambua umuhimu wa mbio za mwenge kwa ajili ya mustakabali wa taifa,ndiyo maana ameamua kutoa mchango wake wa fulana.

"Sisi ni wafanyabiashara ambao kuwepo kwa mazingira mazuri ndani ya taifa kunatupa fursa ya kufanya vizuri na mwenge kwa miaka yote umekuwa nyenzo muhimu ya kuwaunganisha Watanzania bila la kujali dini,kabila ama vipato,"alifafanua.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Hai,Bwana Makunga ameeleza kuwa mwenge wa Uhuru utakuwa wilayani humo Jumatano ya kesho.

Amesema kuwa katika wilaya ya Hai utapitia miradi nane,ambapo kati ya hiyo mitatu itazinduliwa na miwili itafunguliwa wakati mingine mitatu itawekewa mawe ya msingi.

Makunga amefafanua miradi hiyo ni pamoja na bwalo la chakula la shule ya Msingi Kimashuku,Kituo cha afya cha Masama CTC,ofisi ya kijiji cha Mbweera,Kituo cha Maziwa cha Lemira kati,Madarasa matatu shule ya Msingi Mukwasa,Kituo cha mazoezi ya viungo cha Bomang'ombe,Mradi wa vijana wa uhifadhi mazngira Magadini na kituo cha mafunzo cha ufundi chuma kwa vijana Hai mjini.

Amesema kuwa miradi hiyo ina thamani ya shilingi 1,254,365,000/= ambapo mchango wa serikali kuu ni shilingi 479,600,000/=,halmashauri ya wilaya 20,668,000/= na nguvu za wananchi ni shilingi 33,097,000/= na wahisani shilingi 721,000,000.

Amesema kuwa mbio za mwenge za mwaka huu zimebeba ujumbe unaosema "Watanzania ni wamoja" wenye kauli mbiu "Tusigawanywe kwa misingi ya tofauti zetu za dini,itikadi,rangi na rasilimali"

Makunga ameeleza kuwa mwenge huo utapokelewa katika eneo la Maili sita ukitokea wilayani Moshi.

Amesema kuwa baada ya kuwa wilayani Hai kwa siku nzima siku inayofuata wataukabidhi mwenge katika wilaya ya Siha katika eneo la Lawate.


0 comments:

Post a Comment