DC MOSHI ATOA SAA 24 KWA MANISPAA YA MOSHI KUMALIZA UZOAJI WA TAKA MJINI

Posted by Arusha by day and by night On 22:50 No comments


Mkuu wa wilaya ya Moshi,Novatus Makunga akipata maelezo kutoka kwa Afisa wa Manispaa ya Moshi kuhusu uboreshaji wa dampo la kutupia takataka
Kazi ya uzoaji wa takataka ikiendelea kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Moshi
Mkuu wa wilaya ya Moshi,Novatus Makunga akitoa agizo kwa Halmasahauri ya Manispaa ya Moshi kuhakikisha ndani ya saa ishirini na nne wanamaliza tatizo la mrundikano wa taka katika masoko na maeneo mengine
 Na Mwandishi Wetu Moshi

Mkuu wa wilaya ya Moshi,Novatus Makunga ametoa muda wa saa ishirini na nne kwa Halmashauri ya manispaa ya Moshi kuhakikisha inamaliza tatizo la mrundikano wa taka katika maeneo mbalimbali ya mji huo hususani ya masoko.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki baada ya kufanya ziara ya ghafla katika masoko ya Mbuyuni,Manyema na Pasua pamoja na mitaa na Majengo Mississipi na katika dampo la zamani na la sasa katika eneo la Kaloleni

Makunga alisema kuwa kasi ya uzoaji takakata katika mji huo hairidhishi na hivyo kuuagiza uongozi wa manispaa ya Moshi kuongeza muda wa uondoaji wa takataka hasa katika masoko sambamba na ratiba ya kawaida katika mitaa.

Alisema kuwa tayari mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Amos Makalla alishaagizo kwa wilaya zote kuhakikisha zinadhibiti viashiria vyote vitakavyowezesha mkoa huo kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

"Kuwepo kwa taka taka hasa katika maeneo ya masoko ni hatari sana katika kipindi hiki ambacho maeneo mbalimbali yamekumbwa na kipindupindu nchini hivyo ni vyema sasa ni lazima tubanane kwa kila mtu katika eneo lake kuhakikisha anatimiza majukumu yake"alisisitiza Makunga.

Aidha Makunga ametaja hatua zingine ambazo zimeshachukuliwa katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu kuwa ni pamoja na maofisa watendaji wa kata na mitaa kwa usimamizi wa maofisa tarafa kuanza ukaguzi wa nyumba kwa nyumba,maeneo yanayotoa huduma ya chakula na vinywaji pamoja na baa zikiwemo za pombe za kienyeji.

Alisema ukaguzi huo una lengo la kuhakikisha maeneo hayo yana huduma zinasozingatia misingi ya afya bora zikiwemo za vyoo bora na usafi kwa ujumla na akasisitiza kuwa serikali haitasita kuyafunga maeneo ambayo hayakidhi mahitaji na ambayo ni hatarishi kwa afya ya watumiaji

Ugonjwa wa kipindupindu tayari umelipuka katika mikoa mbalimbali ambapo kwa kanda ya kaskazini umezuka katika mikoa jirani ya Arusha na Tanga.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Amos Makalla mapema wiki iliyopita alitoa agizo kwa viongozi wa ngazimbalimbali mkoani humo kuhakikisha ugonjwa huo hauingia katika mkoa wake