SERIKALI YAANZA KUSAMBAZA MSAADA WA CHAKULA WILAYANI HAI
Na Richard Mwangulube,Hai
Serikali wilayani Hai imeanza
kusambaza chakula cha msaada kwa kaya 8,402 zenye upungufu wa chakula wilayani
humo.
Mkuu wa wilaya ya Hai Novatus
Makunga akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake amethibiisha kuanza kwa
zoezi hilo la usambazaji wa mahindi Jumatano iliyopita.
Hata hivyo Makunga amezionya kamati
za maafa za vijiji zinazohusika kuwatambua wahitaji wa msaada huo kuwa na
uadilifu kwa kuhakikisha kaya zinazostahilika msaada huo inaidhinishwa na
mikutano mikuu ya vijiji.
“Maelekezo ya jinsi ya kusimamia
zoezi hilo yapo wazi na wahusika katika ngazo zote za chini yanayafahamu na
tumewapelekea kimaandishi hivyo hatutasita kumchukulia hatua kiongozi yeyote
atakayekiuka muongozi uliotolewa kwa maslahi binafsi,”alisisitiza makunga
Aidha mkuu huyo wa wilaya amezitaka
kaya ambazo zilifanikiwa kuvuna chakula cha kutosha katika msimu uliopita wa
kilimo kuhakikisha zinahifadhi chakula cha kutosha hadi msimu huu wa kilimo
unaotarajiwa kuanza mwezi April.
Makunga ameeleza kuwa msaada huo
mahindi tani 201.6 yametoka ofisi ya waziri mkuu na kupitia katika maghala ya
Wakala wa hifadhi ya chakula nchini(NFRA) yaliyopo jijini Arusha.
Makunga ameeleza kuwa jumla ya kaya
7,561 zitanunua mahindi hayo kwa bei nafuu ya shilingi 50 kwa kilo huku kaya
841 zizokuwa na uwezo zitapewa msaada huo bure.
Ameeleza kuwa kila kaya itapata
kilo 24 ambazo zitatosha kwa matumizi ya miezi miwili.
Makunga ameeleza jumla ya vijiji
kumi na viwili na mitaa sita itanufaika na msaada huo wa chakula.
Amevitaja vijiji hivyo kuwa ni
pamoja na Mtakuja,Tindigani na Sanya Stesheni(kata ya Kia),Mkalama(kata ya
Masama Rundugai),Mbatakero na Kwatito katika kata ya Machame Kusini.
Vijiji vingine ni Longoi na Ngusero(Machame
Weruweru),Usari,Tella na Mulama(kata ya Narumu) na Kitongoji cha Lambo
kilichopo kata ya machame Kaskazini.
Kwa upande wa mitaa iliyopo katika
kata ya Hai mjini ameitaja kuwa ni pamoja na Lerai,Kilimambogo,Mlima
Shabaha,Kambi ya Nyuki,Gezaulole na Kambi ya Raha.