Mtaalamu mtafiti wa kilimo kutoka kituo cha utafiti wa kilimo cha Selian Dkt Peter Matowo akionyesha moja ya mmea wa mahindi uliothiriwa na ugonjwa mpya unaoshambulia mahindi unaofahamika kama Lethal Necrosis Disease}
Mtafiti wa Kilimo Bwana Kitenge akionyesha moja ya mmea uliothiriwa na ugonjwa mpya wa Mahindi katika wilaya ya Hai
Mtaalamu wa kilimo akionyesha mahindi yaliyoathiriwa na ugonjwa hatari wa mahindi wakatika wa mkutano wa wadau wa kilimo wilayani Hai
Na Richard Mwangulebe Hai
Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga amewataka viongozi kuanzia ngazi za vijiji,kata,tarafa mpaka wilayani pamoja na wataalamu wakiwemo maofisa ugani kuhakikisha wanatumia mwezi huu wa mwanzo wa mvua za masika kuwaelimisha wananchi kuhusiana na mbinu za kukabiliana na ugonjwa mpya na hatari wa mahindi.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa agizo hilo wakati anafungua kikao cha dharura cha kuweka mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo kilichowashirikisha watalamu wa kilimo kutoka vituo vya utafiti nchini pamoja na wadau,viongozi wa ngazi mbalimbali,maofisa ugani wa vijiji,viongozi wa dini pamoja na viongozi wa siasa wakiwemo madiwani.
Makunga ameeleza baada ya kikao hicho viongozi wa ngazi ya vijiji wanatakiwa kuitisha mikutano ya vijiji na wale wa kata kukaa katika vikao vya maendeleo ya kata ndani ya wiki mbili ili kuweka mkakati wa kuelimisha wananchi jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huo hatari wa mahindi unaofahamika kama Lethal Necrosis Disease
Aidha amewaagiza wataalamu wa ugani kutumia muda wa siku saba kufanya tathimini ya maeneo yao endapo kuna ugonjwa huo na kuwashilisha taarifa hizo katika vikao vya Halmashauri za vijiji na Kamati za maendeleo za kata na baadaye mwisho wa mwezi katika halmashauri ya wilaya ya Hai.
Ameonya kuwa endapo kila mdau atazembea katika kuhakikisha anatimiza wajibu wake kuwepo kwa ugonjwa huo litakuwa janga kubwa kutokana na idadi kubwa ya wananchi katika wilaya hiyo kutegemea zaidi mahindi kwa matumizi ya family,kipato pamoja na malisho ya mifugo
Makunga pia ameitaka halmashauri ya wilaya kuhakikisha inasambaza kwa wingi vipeperushi vinavyohusiana na ugonjwa huo ili elimu iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi badala ya kuendelea kubaki navyo katika maofisi.
Awali mtaalamu mtafiti kutoka kituo cha utafiti wa kilimo cha Selian cha Arusha Dk Peter Matowo ameeleza kuwa madhara makubwa ya ugonjwa huo ni pamoja na uharibifu shambani unaoweza kufikia asilimia mia moja kwa mimea kufa na kukosa mavuno,magunzi na punje zilizoathirika kuwa na sumu ya magonjwa hatari ya ukungu kwa binadamu na kutofaa kwa malisho ya mifugo.
Ameeleza kuwa ugonjwa huo unaenezwa na virusi na kwamba hauna tiba wala mbegu kinzani na hivyo njia pekee ya kudhibiti ni kwa wakulima kuzingatia kanuni zinazoshauriwa zikiwemo za kung’oa mara moja mimea iliyoathirika,kupiga dawa za kuua wadudu aina ya thrips,beetles,leafhoppers na aphids waenezao ugonjwa huo,kupanda mazao mara tu mvua zinyeshapo pamoja na kilimo cha mzunguko wa mazao.
Ugojwa huo ulianza nchini Marekani mwaka 1976 na kuingia katika nchi za Kenya mwaka 2011 na Tanzania mwaka 2012 na kuenea katika wilaya za mkoa wa Kilimanjaro,Arusha na Mwanza